
Meya wa jiji kuu la Ukraine, Kyiv, Vitali Klitschko, amesema kuwa huenda Ukraine ikalazimika kutoa sehemu ya ardhi yake kama sehemu ya makubaliano ya amani na Urusi, katika kile kinachoonekana kuwa shinikizo linalozidi kuongezeka kutoka kwa Rais wa Marekani, Donald Trump, kuikubali hali hiyo.
“Moja ya uwezekano ni kutoa ardhi. Siyo haki, Lakini kwa ajili ya amani hata kama ni ya muda huenda hilo likawa suluhisho,” amesema Klitschko.
Hata hivyo, bingwa huyo wa zamani wa masumbwi ambaye sasa ni mwanasiasa, alisisitiza kwamba watu wa Ukraine “hawatakubali kamwe uvamizi au udhibiti wa Urusi.”
Kauli yake ilitolewa saa chache tu baada ya shambulizi kubwa la makombora na droni kutoka Urusi mjini Kyiv lililosababisha vifo vya watu 12 na kujeruhi zaidi ya 80, likiwa ni mojawapo ya mashambulizi makubwa zaidi katika miezi ya hivi karibuni dhidi ya mji huo mkuu.
Tangu Rais Vladimir Putin kuanzisha uvamizi wa kijeshi dhidi ya Ukraine mwaka 2022, Urusi inakadiriwa kudhibiti karibu asilimia 20 ya ardhi ya Ukraine kwa sasa.
0 Comments